settings icon
share icon
Swali

Je! Kunayo sababu yoyote ya kuogopa kwenda makaburini?

Jibu


Kwa muda mrefu makaburi yanaonekana kuwa mahali pa kutisha, mara nyingi ni kutokana na asili ya ajabu ya kifo. Makaburi yameandaa mazingira ya visa vingi vya mizimu, mashetani, na uhalifu, na kuwasababisha watu wengi kuogopa makaburi kama mahali pa hatari. Swala la kifo ni jambo la kutatiza kwa watu wengi, lakini Wakristo wanapaswa kuwa na mtazamo tofauti kuhusu kifo na kuhusu kuzuru makaburini.

Inaweza kuwasaidia watu wanaoogopa kwenda makaburini ili kukabiliana na hofu hiyo kwa kuuliza: Je! unadhani ni nini kinaweza kutokea pale? Kando na hadithi za ndoto na mizimu, ni hofu gani ya kweli iliyo makaburini? Yana mabaki ya miili ya binadamu iliyokufa na inayooza ambayo imezikwa futi sita chini ya udongo. Kuna majeneza, mawe ya saruji, alama za shaba, mapambo ya plastiki yaliyoachwa na wapendwa. Mbali na kibanda cha mtunzaji na pengine kanisa dogo au kaburi kubwa na zuri, hakuna kingine pale- na lipi kati ya hayo mambo inayosababisha hofu? Nafsi za waliozikwa zimekwisha hamishwa kwenda katika hatima yao ya kiroho (Luka 16:22).

Kuna uwezekano wa sehemu mbili tu ambapo nafsi zilizowachwa zinaweza kuwa. Kwa Wakristo, “tunalo tumaini na ingekuwa bora zaidi kuuacha mwili huu na kwenda kukaa na Bwana” (2 Wakorintho 5:8). Nafsi za waumini waliozikwa ziko pamoja na Yesu. Wale ambao katika maisha yao ya ulimwengu huu hawakujisalimisha kwa Yesu kama Bwana wako katika “mahali pa mateso” (Luka 16:28). Hakuna roho ya mtu yeyote imeruhusiwa kuelea peke yake kwa uhuru katika maeneo ya makaburi. Waebrania 9:27 inasema, “Kama vile mwanadamu alivyowekewa kufa mara moja tu na baada ya kufa akabili hukumu.” Hakuna uwezekano wa nafsi zilizotuacha kuwa na “makao” makaburini. Hatari halisi na ya kweli iliyoko ni uwezekano wa kujikwaa juu ya jiwe la kaburi na kuguara goti lako.

Wengine ambao wanaelewa kuwa roho za marehemu hazipo kwenye makaburi badala yake wanaweza kuogopa uwepo wa pepo. Mathayo 8:28-34 na Marko 5:1-20 zinataja mtu aliyepagawa na pepo ambaye aliishi makaburini. Hata hivyo, katika kisa hiki, kazi ya mapepo ilihusisha mtu aliye hai. Je! mapepo yanaweza kuishi maeneo ya makaburi? Naam, wanaweza. Lakini hakuna maandiko ambayo yanayoonyesha kuwa mapepo wanafanya kazi zaidi makaburini kuliko maeneo mengine. Zaidi ya hayo, Wakristo hawana chochote cha kuogopa kutoka kwa pepo (1Yohana 4:4).

Wakati mwingine woga wa kwenda makaburini unaweza kuhusishwa na ule uchungu wa kumpoteza mtu na kumbukumbu mahali hapo panaweza ibua. Kwa asili makaburini ni maeneo pa huzuni. Panawakilisha huzuni na kutukumbusha hali ya maisha yetu. Huwa hatupendi kuchochea machungu ya kitambo na makaburi yanaweza kufanya hivyo. Njia moja ya kushinda huzuni inayohusiana na hofu ni kukumbuka kimakusudi nyakati za furaha mlikuwa pamoja na marehemu. Unapotembea kwenye kaburi, kumbuka matukio ya furaha na mazungumzo na mtu huyo. Mshukuru Mungu kwa wakati mwema ulikuwa pamoja na marehemu na jinsi alivyofanya makuu maishani mwako kupitia kwa Rafiki huyo aliyeaga. Mshukuru Mungu kwa sababu ya Yesu an tunaweza kusema, “Kuko wapi, ee mauti, kushinda kwako? Uko wapi, ee mauti, uchungu wako” (1 Wakorintho 15:55)?

Makaburi yatakuwa mahali pa tukio moja la kushangaza zaidi katika historia ya mwanadamu. Wakati Yesu atakaporudi kutupokea katika unyakuo, makaburi yatakua hai. Wathesalonike wa kwanza 4:16 inasema, “Kwa maana Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni, akitoa amri kwa sauti kuu, pamoja na sauti ya malaika mkuu, na sauti ya tarumbeta ya Mungu. Nao waliokufa wakiwa katika Kristo watafufuka kwanza.” Hebu waza juu ya huo wakati! Kwa sisi tunaomjua Kristo, makaburi yatakuwa maeneo ya kusheherekea pindi makaburi yatakapofunguka na miili ya watakatifu kupaa hewani ili kukutana na roho zao. Na baada ya hilo, “ sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili kumlaki Bwana hewani, hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele” (1 Wathesalonike 4:17).

Makaburi ni sehemu ya kiwanja ambacho kimetengwa ili kuwazika wafu, na hakuna sababu zaidi ya kuhofia mahali hapo kuliko mahali kwingine. Wakristo wanaweza pita mahali hapo palipotengenezwa wakiwa na hisia za shukrani kwa yale yote ambayo Mungu amefanya kupitia kwa mtumishi Wake (ona Zaburi 116:15) na hisia za kutarajia kile ambacho Mungu atakifanya katika mahali hapo. Chini ya nyayo zetu mili ya wapendwa wetu inapumzika ambao siku moja watafufuka toka mavumbini kwa mlio wa tarumbeta. Wasioamini wanapaswa kuruhusu hali ya kuogofya ya makaburi iwasukume kutafuta ukweli wa kile kitakachotokea baadaye. Hofu pekee ya kweli itakua ya kumcha Mungu na hukumu Yake. Kwa wasioamini, kwenda makaburini ineweza kuwa tukio la kubadilsha maisha wanapokabiliana na hali ya mauti na kumgeukia Mungu.

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Je! Kunayo sababu yoyote ya kuogopa kwenda makaburini?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries