Swali
Je, Imanueli inamaanisha nini?
Jibu
Imanueli ni jina la kiume la Kiebrania ambalo linamaanisha "Mungu pamoja nasi" au "Mungu yuko nasi." Jina Imanueli linaonekana katika Biblia mara tatu, mara mbili katika Agano la Kale katika kitabu cha Isaya (7:14 na 8:8), na mara moja katika Injili ya Mathayo (1:23).
Katika kitabu cha Isaya, mtoto aliyezaliwa katika wakati wa Mfalme Ahazi alipewa jina la Imanueli kama ishara kwa mfalme kwamba Yuda ingepata utulivu kutoka mashambulio ya Israeli na Shamu: "Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli" (Isaya 7:14). Jina Imanueli ilionyesha ukweli kwamba Mungu angeanzisha uwepo wake wenye mwongozo na ulinzi kwa watu wake katika ukombozi huu. Ishara ya pili na kuu ya unabii wa Isaya kuhusu mtoto aliyeitwa Imanueli ilikua inahusu kuzaliwa kwa Yesu Kristo, masihi wa Israeli.
Miaka mia saba baada ya Mfalme Ahazi, bikira kutoka Nazareti aliyeitwa Mariamu alikuwa ameposwa na Yusufu. Kabla ya kufunga ndoa, malaika alimtokea Yusufu ili kudhibitishwa kwamba Mariamu alikuwa na mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu (Mathayo 1:20-21). Wakati mtoto huyo alipozaliwa, walipaswa kumpa jina Yesu. Huku akielewa utimilifu wa unabii wa Isaya, Mathayo alitangaza ufunuo huu ulioongozwa na Roho: "Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema,Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani,(Mungu pamoja nasi)" Mathayo 1:22-23).
Yesu alitimiza unabii wa Isaya kwa sababu yeye alikuwa "Mungu pamoja nasi"; Alikuwa binadamu kamili na vile vile, Mungu kamili. Yesu alikuja kuishi Israeli na watu wake, kama vile Isaya alivyokuwa ametabiri. Mathayo alimtambua Yesu kama Imanueli, aliyefanyika mtu halisi- muujiza wa Mwana wa Mungu kufanyika mwanadamu na kuishi kati yetu ili aweze kudhihirisha Mungu kwetu. Yesu alikuwa mungu pamoja nasi, aliyedhihirishwa kwa mwili wa kibinadamu (1 Timotheo 3:16).
Injili ya Yohana inaeleza vizuri hali ya kutwaa utu: "Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu. Nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli… Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua" (Yohana 1:14-18).
Katika Yesu, Mungu alitembea nasi na kuzungumza nasi kama alivyofanya na Adamu na Hawa kwenye Bustani ya Edeni. Kuja kwake Yesu Kristo kulionyesha ubinadamu wote kwamba Mungu ni mwaminifu kutimiza ahadi zake. Yesu hakuwa tu ishara ya Mungu pamoja nasi, kama vile mtoto aliyezaliwa wakati wa Ahazi.Yesu alikuwa Mungu pamoja nasi kikamilifu.
Yesu ni Imanueli. Yeye sio ufunuo wa Mungu pamoja nasi kwa kiasi fulani; Yesu ni Mungu pamoja nasi katika utimilifu wake wote: "Maana, ndani yake Kristo katika ubinadamu wake, umo ukamilifu wote wa Mungu" (Wakolosai 2:9). Yesu aliacha utukufu wa mbingu na kutwaa namna ya mtumwa ili achukuane nasi katika udhaifu wetu. (Wafilipi 2:6-11; Waebrania 4:15-16).
Imanueli ni Mwokozi wetu (1 Timotheo 1:15). Mungu alimtuma Mwanawe kuishi kati yetu na kufa kwa ajili yetu msalabani. Kupitia damu ya Kristo iliyomwagika, tunaweza kupatanishwa na Mungu (Warumi 5:10; 2 Wakorintho 5:19; Wakolosai 1:20). Tunapozaliwa katika Roho wake, Kristo anakuja kuishi ndani yetu (2 Wakorintho 6:16: Wagalatia 2:20).
Imanueli wetu atakuwa nasi milele. Baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu, kabla ya Yesu kurudi kwa Baba, aliahidi: "Mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari" (Mathayo 28:20; Tazama pia Waebrania 13:5). Hakuna chochote kitakachotutenganisha na Mungu na upendo wake kwetu katika Kristo (Warumi 8:35-39).
English
Je, Imanueli inamaanisha nini?