settings icon
share icon
Swali

Je! Ninaweza kufanya nini wakati sihisi upendo wowote kwa Mungu?

Jibu


Kwanza, swali muhimu: je, umezaliwa mara ya pili? Umemwamini Bwana Yesu kwa wokovu wako? Ikiwa ndivyo, uadui kati yako na Muumba wako umetoweka, na umeingia katika uhusiano salama na wenye upendo pamoja na Mungu. Ikiwa huna imani katika Kristo, basi huna uhusiano na Mungu (Yohana 14:6).

Hisia huja na kuondoka, na huenda “usihisi” upendo kwa Mungu kila wakati. Mioyo huwa inapoa na hata wale Wakristo waliomoto huwa na matatizo katika kudumisha upendo na huduma yao kwa Mungu. Ilibidi Kanisa katika Efeso kukumbushwa na Kristo: “Umeuacha upendo wako wa kwanza” (Ufunuo 2:4). Ukosefu wa hisia za upendo, hata hivyo, haimaanishi kuwa uhusiano umeisha. Mungu habadiliki; Upendo wake ni wa kudumu.

Ni maneno yamesemwa mara kwa mara lakini, usikate tamaa! Jua kwamba Mungu anakupenda na anatamani uwe na maisha tele na yenye amani ndani ya vigezo vya mapenzi yake. Mungu ni Baba mwenye upendo, huruma na anayekuangalia kwa upendo mkuu. Andiko la 2 Wakorintho 1:3 linamfafanua Mungu kuwa “Baba wa huruma na Mungu wa faraja yote.” Anakupenda sana na anatamani kukusaidia katika wakati huu wa majaribu ya kuhisi kutengwa naye.

Msingi wa uhusiano wetu na Mungu ni upendo. Alitupenda na akamtuma Mwanawe (Yohana 3:16), na mwitikio wetu kwa upendo wake ni kumpenda Yeye (1 Yohana 4:19) na kumtumikia pia. Si huduma kwa sababu ya wajibu, bali kwa upendo wa kweli Kwake na kwa kuwa Yeye ni Mungu. Mapenzi ya Mungu sio kwamba tujitoe “si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu” (2 Wakorintho 9:7). Kwa hivyo unawezaje kuwa mtu “anayetoa kwa moyo mkunjufu” ambaye ameutoa moyo wake kwa hiari kwa Mungu?

Tafakari juu ya mwenendo wako umbali huu
Je, Wakristo wanapaswa kuhisi wachangamfu kwa Mungu nyakati zote? La. Sisi sote tuna mabonde na majangwa katika matembezi yetu na kuhisi kila aina ya mihemko katika sehemu mbalimbali za maisha yetu-kama vile tunavyofanya katika mahusiano mengine. Katika kufufua upendo wako kwa Mungu, anzia mwanzo kabisa. Tafakari ni wapi na ni jinsi gani mwenendo wako na Yeye ulianza. Uliokoka lini? Kwa nini uliokolewa? Ulihisi nini ulipoanza kugundua Mungu ni nani? Je, ni namna gani Yesu amajifunua kwako katika maisha yako ya kila siku tangu wakati huo? Ni mambo gani maishani Mungu amekushindia? Fikiria ushindi uliopita (1 Samweli 7:12) na nyakati zile ambapo ulihisi hamu kubwa na hamu ya Mungu katika maisha yako.

Omba
Tumia wakati mzuri na Mungu. Mjue zaidi. Kumjua ni kumpenda. Muulize Mungu akuzidishie shauku yako kwake. Muulize akujaze na Roho Wake na kuamsha tena uthamini wake wa tabia Yake. Endelea kujitiisha kwa Roho Mtakatifu na kukiri kwa Mungu kwamba huwezi kushinda mapambano haya peke yako-hakuna hata mmoja wetu anayeweza. Tunapoomba usaidizi kutoka kwake, kila mara Yeye hutusikia! Zaburi 18:6 inasema, “Katika shida yangu nalimwita Bwana, nilimlilia Mungu wangu anisaidie. Kutoka hekaluni mwake alisikia sauti yangu, kilio changu kikafika mbele zake, masikioni mwake.”

Soma Maandiko
Katika nyakati ambazo huhisi chochote kwa Mungu, kusoma Neno la Mungu kunasaidia kukumbuka jinsi anavyohisi kukuhusu. Chimbua Maandiko kadri uwezavyo huku ukishughulika na hisia hizi za kutopendezwa. Neno la Mungu kweli ni “ taa ya miguu yangu na mwanga katika njia yangu” (Zaburi 119:105). Jaribu kusoma zaburi moja kila siku. Kitabu cha Zaburi kinatia moyo sana na kina sala nyingi ambazo unaweza kujihusisha nazo, ukizingatia hali yako ya sasa. Ni katika Neno kwamba Mungu anajidhihirisha Mwenyewe na mapenzi yake kwako.

Tafuta ushauri wa Kikristo
Hii ni muhimu hasa ikiwa una hamaki au kumkasirikia na Mungu kwa sababu fulani. Ni vigumu kuhisi upendo kwa mtu wakati una hasira naye. Ikiwa kuna tatizo la hasira, umejisikia hivi kwa muda gani? Je, unaweza kuhusisha hisia zako kwa hali fulani? Je, kuna kitu kinachosaidia kupunguza hisia zako au kubadilisha mtazamo wako kwa muda? Ushauri wa kibiblia unaweza kukusaidia kutatua masuala mahususi. Kupitia mchakato wa uponyaji, ukiongozwa na mchungaji au mshauri mwingine, unapaswa kuwa na uwezo wa kuacha hasira na maumivu, na mtazamo wako wa Mungu unapaswa kubadilika na kuwa bora.

Tafuta mnasihi mcha Mungu
Hakika, kuna mtu unayemjua ambaye anampenda Bwana na ambaye furaha yake ya Kikristo ni dhahiri. Uliza mtu huyu kukutana nawe mara kwa mara. Tumia wakati pamoja, jifunzeni Biblia pamoja, ombeni pamoja. Uliza maswali kuhusu matembezi ya kiroho ya mshauri wako na jinsi unavyoweza kumpenda Bwana zaidi. Rafiki huyu anaweza kukutia moyo katika safari yako.

Jiunge na kanisa lililo karibu nawe
Mungu anakusudia maisha ya Kikristo yawe ya ushirika. Ndiyo maana analiita kanisa “mwili” wa Kristo (Warumi 12:5). Kuna fursa nyingi za kumtumikia Bwana kupitia kanisa lako na watu wengi wanaoweza kukuhimiza, kukuunga na kukutia moyo.

Mungu ataendelea kukupenda sana! “Nami ninaomba kwamba ninyi mkiwa wenye mizizi tena imara katika msingi wa upendo, mwe na uwezo wa kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, urefu, kimo na kina upendo wa Kristo, na kujua upendo huu unaopita fahamu, ili mpate kujazwa na kufikia kipimo cha ukamilifu wote wa Mungu” (Waefeso 3:17-19).

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Je! Ninaweza kufanya nini wakati sihisi upendo wowote kwa Mungu?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries