settings icon
share icon
Swali

Je, Biblia inasema nini kuhusu kuinama au kupiga magoti katika maombi?

Jibu


Zaburi 95:6 inasema, “Njooni, tusujudu, tumwabudu, tupige magoti mbele za Bwana Muumba wetu.” Kuinamana na kupiga magoti kwa muda mrefu kumehusishwa na ibada na heshima (ona 2 Mambo ya Nyakati 6:13; Zaburi 138:2; Danieli 6:10). Kwa kweli, neno la Kiebrania linalotafsiriwa “kuabudu” kwa kweli linamaanisha “kuinama.” Lakini kuinama au kupiga magoti ndio mkao/hali pekee tunaopaswa kuuchukua katika kuabudu au kusali?

Tukio la kwanza lililonakiliwa katika Bibilia la kuinama kwa heshima liko katika Mwanzo 18:2 wakati wageni watatu wa mbinguni walipomjia Abrahamu. Alijua walimwakilisha Mungu, naye akainama chini kwa kuwakaribisha. Vizazi vichache baadaye, Farao, mfalme wa Misri, aliamuru Wamisri wote kumwinamia Yusufu kama ishara ya heshima kwa mtumwa wa zamani aliyepandishwa cheo na kuwa wa pili (Mwanzo 41:42-43). Kwa hivyo, mapema sana katika historia ya wanadamu, kuinama au kupiga magoti kulikuja kuwakilisha kuchukua nafasi ya unyenyekevu mbele ya mtu wa maana zaidi.

Kuinama na kupiga magoti mbele ya watawala na miungu ya uongo ilikua jambo la kawaida wakati Mungu alipompa Musa Sheria. Mungu alitaka kuweka mipaka mipya kuhusu ibada inayodaiwa kwake. Amri ya pili inasema, “Usijitengenezee sanamu katika umbo la kitu .... Usivisujudie wala kuviabudu; kwa kuwa Mimi, Bwana Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu” (Kutoka 20:4-5). Mungu amejiwekea aina yoyote ya ibada, na kusujudu Yeye mwenyewe, na kuinama mbele ya mtu yeyote au kitu chochote kama aina ya ibada imekataliwa. Katika Ufunuo 19:10 Yohana anaanguka miguuni pa malaika aliyekuwa akimfafanulia maono, lakini mara moja malaika anamrekebisha: “Usifanye hivyo! Mimi pia ni mtumishi mwenzako pamoja na ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Mwabudu Mungu!”

Kuinama na kupiga magoti hakukuwa namna pekee ya mikao iliyokubaliwa na waabudu katika Biblia. Musa na Haruni walianguka kifudifudi mbele za Bwana, na utukufu wake ukawafunika (Hesabu 20:6). Ezekieli alianguka kifudifudi kwa huzuni, akimlilia Bwana, na Bwana akamjibu (Ezekieli 11:13-14). Walawi walipaswa “kila asubuhi kumshukuru na kumsifu Bwana. Iliwapasa pia kufanya hivyo jioni” (1 Mambo ya Nyakati 23:30). Mfalme Daudi “akaingia ndani, akaketi mbele za Bwana” (2 Samweli 7:18). Yesu “aliinua macho Yake kuelekea mbinguni” wakati alifanya sala yake refu iliyonakiliwa (Yohana 17), na Paulo akawahimiza “wanaume wasali wakiinua mikono mitakatifu pasipo hasira wala kugombana” (1 Timotheo 2:8). Kulingana na Biblia, kunayo zaidi ya mkao mmoja wa kuabudu na kusali.

Ingawa uwakilishi wa kimwili wa ibada ni muhimu, na nafsi yetu yote inapaswa kushiriki katika kumbwabudu Mungu, mkao wa mioyo yetu ni muhimu zaidi kuliko mkao wa miili yetu. Wakati mkao wa mioyo yetu ni unyenyekevu na heshima, miili yetu kila mara hutamani kueleza hilo kwa njia zinazoonekana. Kupiga magoti, kuinama, kusujudu, kuinamisha vichwa na kuinua mikono yetu zote ni hali za kimwili za kuonyeshea nia ya mioyo yetu. Bila shaka, bila mkao wa moyo unaolingana vitendo vya kimwili ni maonyeshesho tupu. Zaburi 51:17 inaeleza kwa ufasaha tamanio ya Mungu kwa ajili ya ibada yetu: “Bali dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika, moyo uliovunjika wenye toba, Ee Mungu, hutaudharau.”

Ibada ya kweli ni mtindo wa maisha, si shughuli. Ingawa nyakati zilizotengwa za ushirika wa kina na Mungu ni muhimu kwa afya yetu ya kiroho, tunaambiwa pia “kuomba bila kukoma” (1 Wathesalonike 5:17). Miili yetu inapaswa kuwa dhabihu iliyo hai (Warumi 12:1-2) na mioyo yetu imejawa na “zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni, mkimwimbia na kumsifu Bwana mioyoni mwenu, siku zote mkimshukuru Mungu Baba kwa kila jambo katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo” (Waefeso 5:19-20). Mioyo yetu inaweza endelea kuwa katika hali ya kuabudu na kusali, hata wakati tuko katika shughuli zetu za siku. A. W. Tozer aliandika, “Lengo la kila Mkristo linapaswa kuwa kuishi katika hali ya ibada isiyovunjika.” Wakati hilo ndilo lengo la maisha yetu, kupiga magoti, kuinama, kulala kifudifudi, na kutembea barabarani yote ni mikao ya sala na ibada ambazo zinampendeza Mungu.

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Je, Biblia inasema nini kuhusu kuinama au kupiga magoti katika maombi?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries