Swali
Ina maana gani kwa Mkristo kukua katika imani?
Jibu
Tumeagizwa katika Maandiko “Bali kueni katika neema na katika kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo (2 Petro 3:18). Kukua huku ni kukua kiroho, kukua katika imani.
Wakati tunampokea Kristo kama Mwokozi, tunazaliwa mara ya pili kiroho katika familia ya Mungu. Lakini kama vile mtoto mchanga anavyohitaji maziwa ili kukua vizuri, vile vile Mkristo mchanga anahitaji chakula cha kiroho ili kukua. “Kama watoto wachanga, waliozaliwa sasa, yatamanini maziwa ya kiroho yasiyochanganywa na kitu kingine chochote, ili kwa hayo mpate kukua katika wokovu, ikiwa kweli mmeonja ya kwamba Bwana ni mwema” (1 Petro 2:2-3). Maziwa yanatumika katika Agano Jipya kama mfano wa kile ambacho ni muhimu kwa maisha ya Kikristo.
Kadri mtoto anavyokua, lishe yake hubadilika na kujumuisha pia vyakula vigumu. Ukitilia hili maanani, soma vile mwandishi wa Waebrania alivyowahimiza Wakristo: “Kwa hakika, ingawa mpaka wakati huu ingewapasa kuwa walimu, bado mnahitaji mtu wa kuwafundisha tena hatua za awali za kweli ya Neno la Mungu. Mnahitaji maziwa, wala si chakula kigumu! Kwa maana yeyote aishiye kwa kunywa maziwa bado yeye ni mtoto mchanga, hana ujuzi katika mafundisho kuhusu neno la haki. Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu wazima, ambao kwa kujizoeza wamejifunza kupambanua kati ya mema na mabaya (Waebrania 5:12-14). Paulo aliona tatizo sawia katika waumini wa Korintho; hawakuwa wamekua katika imani yao, na angewapa tu “maziwa” kwa sababu hakuwa tayari kula chakula kigumu (I Wakorintho 3:1-3).
Ulinganisho kati ya mtoto wa kibinadamu na mtoto wa kiroho unatofautiana tunapotambua jinsi kila mtoto anavyokomaa. Mtoto wa kibinadamu analishwa na wazazi wake na ukuaji ni wa asili. Lakini mtoto wa Kikristo atakua kadri anaposoma na kutii kimakusudi na kutumia Neno katika maisha yake. Ukuaji unamtegemea yeye mwenyewe. Kuna Wakristo ambao wameokoka miaka mingi lakini lakini bado wao ni watoto kiroho. Hawawezi kuelewa ukweli wa ndani wa Neno la Mungu.
Lishe ya Mkristo inapaswa kuwa na nini? Neno la Mungu! Ukweli unaofunzwa katika Biblia ni chakula bora cha Mkristo. Petro aliandika kuwa Mungu ametupa kila kitu tunachohitaji maishani kupitia ukuaji wetu katika kumjua Mungu. Soma kwa makini 2 Petro 1:33-11 ambapo Petro anaorodhesha sifa za tabia zinazohitajika kuongezwa kwenye hatua yetu ya mwanzo wa imani ili tupate kukomaa na kukaribishwa katika ufalme wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.
English
Ina maana gani kwa Mkristo kukua katika imani?