settings icon
share icon
Swali

Ikiwa Yesu aliwakashifu Mafarisayo kwa kuomba kwa sauti, je! tunapaswa kuomba kwa sauti?

Jibu


Kuna marejeleo mengi katika Agano Jipya kwa maombi ya hadhara ambayo hayakubaliki, na ni kweli kwamba Yesu alikashifu namna ya kuomba ya Mafarisayo. Lakini Yesu Mwenyewe aliomba kwa sauti wakati mwingine (ona Yohana 17), kama vile walivyofanya mitume (Matendo 8:15; 16:25; 20:26). Matendo 1:14 inasema, “Hawa wote waliungana pamoja katika maombi. Pamoja nao walikuwepo wanawake kadha, na Maria mama yake Yesu, pamoja na ndugu zake Yesu.” Kisha katika mstari wa 24, mitume waliomba pamoja ili kumchagua atakaye chukua nafasi ya Yuda kati ya wale kumi na wawili. Walikuwa wakiomba pamoja na kwa sauti kubwa. Kwa hivyo dhambi haikuwa katika hali ya kuomba kwa hadhara au kwamba watu wangeweza kuwasikia.

Katika Luka 18:10-14, Yesu anatoa mfano huu: “Watu wawili walikwenda Hekaluni kusali, mmoja wao alikuwa Farisayo na mwingine alikuwa mtoza ushuru. Yule Farisayo, akasimama, akasali hivi na kuomba kwake mwenyewe: ‘Mungu, nakushukuru kwa sababu mimi si kama watu wengine ambao ni wanyangʼanyi, wadhalimu, na wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma, na natoa sehemu ya kumi ya mapato yangu.’ “Lakini yule mtoza ushuru akasimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua uso wake kutazama mbinguni, bali alijipigapiga kifuani na kusema: ‘Mungu, nihurumie, mimi mwenye dhambi.’ “Nawaambia, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amehesabiwa haki mbele za Mungu zaidi ya yule Farisayo. Kwa maana yeyote ajikwezaye atashushwa, na yeyote ajishushaye atakwezwa.” Dhambi ya Mafarisayo haikuwa katika kuomba hadharani bali katika roho ya majivunuo.

Baadaye Yesu anasema, “Jihadharini na walimu wa sheria. Wao hupenda kutembea wakiwa wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa kwa heshima masokoni. Hupenda kukaa kwenye viti vya mbele katika masinagogi, na kukaa kwenye nafasi za heshima katika karamu. Wao hula nyumba za wajane, na ili waonekane kuwa wema, wanasali sala ndefu. Watu kama hawa watapata hukumu iliyo kuu sana” (Luka 20:46-47). Hapa dhambi haiko katika maombi yanayosikika bali katika unafiki wao. Yesu alikashifu unafiki wa kuonekana kuwa na uhusiano na Mungu huku wakiwakandamiza watu hao hao Yeye anawapenda.

Katika Mathayo 6:5, Yesu anasema, “Nanyi msalipo, msiwe kama wanafiki, maana wao hupenda kusali wakiwa wamesimama katika masinagogi na kando ya barabara ili waonekane na watu. Amin nawaambia, wao wamekwisha kupata thawabu yao.” Hapa pia Yesu hakashifu dhana kuwa watu waliomba kwa sauti, lakini walikuwa na ile hali ya mwonekano wa hadhara kwa manufaa yao wenyewe. Nia yao-ya kuonekana na watu-ndio ilikuwa shida. Maombi kama hayo, sio maombi ya kweli, bali maneno tupu ambayo yamekusudiwa kwa masikio ya watu wengine (Waebrania 10:22). Mithali 15:29 inasema, “Bwana yuko mbali na waovu, bali husikia maombi ya wenye haki.”

Katika Waefeso 5:20, Paulo analiagiza kanisa “siku zote mkimshukuru Mungu Baba kwa kila jambo katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo.” Maombi ya pamoja ni njia mojawapo kanisa linaweza kumwabudu Mungu na kuhimizana. Kile Yesu anakashifu ni kiburi na unafiki. Kwa mtu ambaye kwa wazi hamtii Mungu na anaongoza maombi ya hadhara kana kwamba yeye ana mengi ya kujivunia ndio aina ya unafiki ambao Yesu anakashifu. Kutumia maombi ya hadhara kama chombo cha kujivunia au kuwafurahisha wengine ni makosa. Lakini kwa kuwa sala ya dhadi kutoka kwa moyo wa unyenyekevu daima inakaribishwa na Mungu na inaweza kuwa faraja kwa wale wanaoisikia (Zaburi 51:17).

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Ikiwa Yesu aliwakashifu Mafarisayo kwa kuomba kwa sauti, je! tunapaswa kuomba kwa sauti?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries