Swali
Je! Hesabu 32:23 inamaanisha nini inaposema, ‘kuweni na hakika kuwa dhambi yenu itawapata’?
Jibu
Hesabu 32:23 inasema, “kuweni na hakika kuwa dhambi yenu itawapata.” Hii ni tahadhari ya kushangaza, haswa ikiwa inasomwa pekee yake. Kwa hivyo tutaangalia muktadha wake, haswa sura nzima ya Hesabu 32, kisha tuone kile kingine ambacho Biblia inasema juu ya mada ya dhambi yetu “kutupata.” Kauli “kuweni na hakika kuwa dhambi yenu itawapata” imewekwa katika kukamilika kwa msafara wa Israeli kutoka Misri. Baada ya kutanga-tanga nyikani kwa miaka 40, hatimaye makabila ya Israeli yalikuwa yakijitayarisha kuvuka Mto Yordani na kuingia katika Nchi ya Ahadi. Wanaume wenye umri wa kujiunga na jeshi kutoka makabila yote kumi na mawili walitakiwa kusaidia kila kabila kushinda eneo walilopewa, jukumu ambalo lingehusisha wakati mwingi na magumu.
Kabla ya Waisraeli kuvuka Yordani, makabila ya Gadi na Reubeni yalifanya ijulikane kuwa walipapenda pale walipokuwa, mashariki mwa Yordani. Nchi hiyo ilikuwa bora kwa kufuga ng’ombe (Hesabu 32:1), na viongozi wa makabila hayo walimwendea Musa ili wapate ruhusa ya kukaa upande wa mashariki, badala ya Kanaani. Hapo mwanzo Musa alisema “la”: “Je, watu wa nchi yenu watakwenda vitani wakati ninyi mmeketi hapa?” (aya ya 6). Kisha akawashutumu kwa kutotamani kuingia katika Nchi ya Ahadi, kama kizazi kilichotangulia kilivyofanya: “Hivi ndivyo baba zenu walivyofanya” (aya ya 8). Naye akawakumbusha kwamba ilikuwa ni dhambi hiyohiyo iliyosababisha hasira ya Bwana kuwaka juu yao kwa muda wa miaka 40, na akawaonya kwamba walihatarisha kuleta uharibifu juu ya taifa zima tena (mistari ya 13-15).
Lakini Gadi na Reubeni walikuwa na nia tofauti, kama walivyoeleza. Walimwomba Musa kama wangeweza kuacha mifugo na familia zao nyuma katika makazi hayo, huku wanaume wakiwa wamejihami na kwenda vitani Kanaani. Baada ya kuhakikishiwa kwamba hawakuwaacha Waisraeli wenzao, Musa alikubali ombi lao. Aliwaambia lazima wapigane hadi nchi itakapokuwa imeshidwa, na ndipo wangeweza kurudi kwenye mali yao mashariki mwa Yordani. Kisha Musa akongeza onyo hili: “Lakini mkishindwa kufanya hili, mtakuwa mnatenda dhambi dhidi ya Bwana; nanyi kuweni na hakika kuwa dhambi yenu itawapata” (Hesabu 32:23).
Wakati Musa alisema, “kuweni na hakika kuwa dhambi yenu itawapata,” hakumaanisha, “Kila mtu atajua kuhusu dhambi yao.” Ikiwa makabila ya ng’ambo ya Yordani yangeshindwa kutimiza ahadi yao, ingekuwa dhambi dhidi ya Bwana na taifa zima, na dhambi yao ingekuwa dhahiri kwa wote. Badala yake, onyo la Musa kwamba waweze kuwa na uhakika kwamba dhambi yao itawapata inadokeza asili ya ajabu-lakini ya kweli kuhusu dhambi.
Katika sehemu nyingi katika Biblia, dhambi inafafanuliwa kwa maneno ambayo hufanya ionekane kana kwamba ni kiumbe hai chenye akili na mapenzi yake yenyewe. Mungu kimafumbo anamuonya Kaini kwamba “dhambi inakuvizia mlangoni mwako, inakutamani wewe, lakini inakupasa uishinde” (Mwanzo 4:7). Yakobo anaelezea kitamathali jinsi watu, “wanapovutwa na kudanganywa na tamaa zao wenyewe zilizo mbaya. Basi ile tamaa mbaya ikishachukua mimba, huzaa dhambi, nayo ile dhambi ikikomaa, huzaa mauti” (Yakobo 1:14-15). Paulo katika Warumi 7:14-25, anaelezea dhambi kana kwamba ilikuwa kiumbe aliyeishi ndani yake, inayomfunga kinyume na mapenzi yake na kumfanya afanye kile ambacho yeye mwenyewe anachukia na kulaani: “Si mimi tena nifanyaye hivyo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu” (aya ya 20).
Katika usemi “kuweni na hakika kuwa dhambi yenu itawapata” siri ya dhambi inafafanuliwa. Asili ya dhambi ni kwamba, iwe wengine watagundua dhambi yako au la, dhambi yako itakutambulisha.” Hauwezi toroka matokeo. Dhambi inabeba ndani yake uwezo wa kumlipa mwenye dhambi, na malipo ya dhambi ni jehanamu. Usifikirie hata kujihusisha na dhambi. Haiwezi kufungwa, kutorokwa, au kutikiswa. Haijalishi unafikiri uko salama kiasi gani, ikiwa wewe ni mwenye dhambi, dhambi yako itakupata.
Onyo la Musa kwa makabila ya Israeli, “kuweni na hakika kuwa dhambi yenu itawapata” linarudiwa na Paulo: “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. Apandaye kwa mwili, katika mwili wake atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele” (Wagalatia 6:7-8). Njia pekee ya kutoroka matokeo ya dhambi ni kusamehewa dhambi zako kwa imani katika kifo na ufufuo wa Kristo (Warumi 10:9; 1 Yohana 2:2; Ufunuo 1:5).
English
Je! Hesabu 32:23 inamaanisha nini inaposema, ‘kuweni na hakika kuwa dhambi yenu itawapata’?