Swali
Jinsi gani naweza kuepuka kuwezesha dhambi ya mtu mwingine?
Jibu
Kuwezesha dhambi ni kuimarisha mtu mwingine kuendelea kutenda dhambi, kuongeza uwezo wake wa kutenda dhambi, au kuifanya kuwa rahisi kwake kutenda dhambi. Katika msimamo wetu wa haki, tunataka kuepuka kuwezesha dhambi za wengine. Mahusiano ya kibinadamu yanaweza kuwa magumu, na kuna hali nyingi ambazo zinaweza kusababisha ushirika wa hiari katika dhambi za mtu mwingine. Katika ndoa, mwenzi mmoja anaweza kuvutwa katika dhambi kwa jitihada za kumridhisha mwenzi mwingine. Marafiki na familia ni njia ambazo shetani mara nyingi hutumia kutuvutia kushiriki katika dhambi ambazo kwa kawaida tungezikwepa (1 Wakorintho 15:33; Mithali 22:24). Hata hivyo, hakuna mtu ambaye ako na uwezo wa kumfanya mtu mwingine atende dhambi. Dhambi ni hali ya moyo ( Mathayo 15:18-19). Na kila mmoja wetu ako na jukumu kwa maamuzi tunayofanya na hali ya mioyo yetu wenyewe (Warumi 14:12; Mathayo 12:36).
Kuwezesha dhambi ya mtu mwingine ni sawa na kushiriki kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika dhambi hiyo, na 1 Timotheo 5:22 inasema, “Usimwekee mtu mikono kwa haraka, wala usizishiriki dhambi za watu wengine. Ujilinde nafsi yako uwe safi.” Ikiwa Biblia ina amri, tuko na uwezo wa kuitii. Mara nyingi hatufahamu kwamba tuna haki na wajibu wa kuweka mipaka ya kibinafsi ambayo inamtukuza Mungu. Kujifunza kuweka mipaka imara kwa ajili yetu ni muhimu katika kuishi maisha yenye ushindi ambayo Yesu anatutakia (Yohana 10:10; Warumi 8:37). Mipaka inatufafanulia wajibu wetu penye unaanzia na penye unamalizikia. Tunapojua mipaka hiyo, sisi ndio wenye jukumu la kuitekeleza. Kwa mfano, ikiwa rafiki anasisitiza kuwa uendeshe gari la kutorokea katika wizi, haufai kufanya uamuzi. Uamuzi ulifanywa wakati uliamua kumfuata Kristo kwanza. Yesu anasema kuiba ni makosa, kwa hivyo hautawezesha wizi. Kushiriki katika dhambi si chaguo kwa Mkristo ( Warumi 6:1-2; 1 Yohana 3:9).
Kuepuka dhambi kunahitaji kwamba tunatafuta hekima kutoka kwa Mungu. Kwa bahati nzuri, tunaahidiwa katika Yakobo 1:5, “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.” Tunapopokea hekima ya Mungu kuhusu hali fulani, jukumu letu ni kwenda mbele kwa msingi wa hekima hiyo. Mojawapo ya njia za kupata ujasiri katika kufanya maamuzi sahihi ni kujiuliza tungeweza kufanya nini kama Yesu angekuwa anasimama karibu nasi. Ikiwa hatutaweza kwenda mbele na Yesu, basi huo sio uamuzi sahihi, bila kujali ni nani anatuhimiza kushiriki.
Njia moja ambayo tunawezesha dhambi za wengine ni kwa kuwaokoa kotoka kwa matokeo yao. Mungu hutumia matokeo ya matendo yetu kutufundisha hali fulani ambayo hatungejifunza vinginevyo. Wakati Mkristo anawaruhusu marafiki zake kumshawishi kwenda mahali anajua itapelekea kufanya tabia za dhambi, anashiriki katika dhambi za wengine. Tunawapa wengine uhuru wa kufanya uchaguzi wao wenyewe, lakini lazima pia tuwaruhusu wavune matokeo ya uchaguzi huo ( Wagalatia 6:7). Mara nyingi tunawawezesha wengine kutenda dhambi kwa sababu ya hisia za uongo za huruma au kwa sababu tunataka kuwa na umuhimu kwao.Kuna nafasi ya neema, lakini kwa kuwalinda mara kwa mara kutokana na matokeo ya kawaida ya dhambi, tunamwibia mtu huyo hekima ambayo Mungu angetaka kumpatia. Sio rahisi kuona mpendwa akikabiliana na shida, lakini mara nyingi shida ndio Mungu anataka kutumia kufundisha somo muhimu la maisha.
Kuwezesha dhambi mara nyingi hutokea kwa njia ndogo ndogo. Tunapokubali kusikiliza uzushi badala ya kukemea, tunawezesha dhambi. Tunapotoa pesa kwa rafiki ambaye tunashuku anaitumia kwa mambo mabaya, tunawezesha dhambi. Hata tunapowasaidia kwa majukumu muhimu, bado tunaweza kuwawezesha kutenda dhambi wakati tunajua kwamba rafiki yetu anahitaji msaada kwa sababu amepoteza pesa yake kwa kamari/madawa/kujitosheleza na vitu vya kimwili/n.k. Kuwaalika marafiki kuja kuangalia sinema pamoja nasi wakati tunajua kwamba inaweza kuchochea matatizo yao ya dhambi inatufanya kuwa wawezeshaji wa dhambi. Hatuhitaji kuwa walinzi wa dhambi za wengine, lakini tunapojua shida zao, hatupaswi kuwaalika kwenye hali zenye majaribu; badala yake, tunapaswa kuwa pamoja nao ili kuwasaidia.
Kama vile wengine wana uhuru wa uchaguzi wao, sisi pia tuna uhuru wa kuchagua, na tunaweza kuchagua kutoshiriki katika dhambi za wengine. Mara nyingi tunajikuta tukivutwa kwenye dhambi za mtu mwingine kwa sababu tunahofia kupoteza uhusiano na mtu huyo. Kwa kufanya hivyo, tumemruhusu mtu huyo achukue nafasi ya Mungu mioyoni mwetu. Tunapokuwa na tamaa ya mtu mwingine inayozidi tamaa ya Mungu, tumekwishaanguka katika ibada ya sanamu ( Kutoka 20:3; 34:14). Tunaweza kuepuka kuwezesha dhambi ya mtu mwingine kwa kufanya uamuzi wa mwisho juu ya nani anayeongoza maisha yetu. Ikiwa tumeweka maisha yetu kwa Kristo, basi Yeye ndiye mamlaka ya mwisho kuhusu uamuzi wowote (2 Wakorintho 10:15; Matendo ya Mitume 5:29).Ikiwa Yesu hangefanya iwe rahisi kwa mtu kutenda dhambi, basi sisi pia hatupaswi kufanya hivyo.
English
Jinsi gani naweza kuepuka kuwezesha dhambi ya mtu mwingine?