settings icon
share icon
Swali

Je! Biblia inasema nini kuhusu ubaguzi wa umri?

Jibu


“Ubaguzi wa umri” kwa ujumla inaeleweka kuwa ubaguzi dhidi ya kikudi fulani cha umri. Ingawa ubaguzi wa umri unaweza kulenga kikundi chochote cha umri, ubaguzi huwa unalenga wale walio na umri mkubwa zaidi. Ubaguzi wa umri unaweza kuathiri vibaya matarajio ya kazi ya mtu, upatikanaji wa huduma za afya, na jinsi mtu huyo na mawazo yake na maoni yake yanavyotambuliwa.

Ingawa ubaguzi wa umri ni neno la kisasa ambalo halipatikani katika Biblia, Maandiko bado yana mengi ya kusema juu ya suala hilo. Kwanza kabisa, tutaona kwamba Neno la Mungu linashutumu ubaguzi wa aina yoyote, hasa miongoni mwa waumini. Yesu anaonyesha kwamba amri kuu zaidi ni kumpenda Bwana kwa mioyo yetu yote na kuwapenda jirani zetu kama tunavyojipenda sisi wenyewe (Marko 12:30-31). Kama waumini, sisi sote ni sawa machoni pa Mungu, na kila mtu anastahili heshima sawa (ona Wagalatia 3:27-28; Yakobo 2:2-4). Bwana Mwenyewe “hana upendeleo” (Matendo 10:34; Warumi 2:11).

Pia kuna kanuni za kibiblia ambazo huzungumzia hasa ubaguzi wa umri. Biblia inafundisha kwamba wazee wanapaswa kuheshimiwa sana. Umri wao haufai kuonekana kuwa mbaya bali ni kitu kinachowatofautisha kwa sababu ya hekima waliyokusanya kwa miaka mingi. Wazee hufundisha kizazi kipya (ona Tito 2:3-4); kitabu kizima cha Mithali kimetolewa kama maagizo ya baba kwa mwanawe (ona Mithali 1:8). “Mvi ni taji ya utukufu; hupatikana kwa maisha ya uadilifu” (Mithali 16:31), na “Utukufu wa vijana ni nguvu zao, mvi ni fahari ya uzee” (Mithali 20:29). Kujifunza kutoka kwa mzee mwadilifu ni heshima na faida.

Wakati Mungu alitoa Sheria kwa watu wake, alimwagiza Musa awaambie, “Uwapo mbele ya mzee, simama ili kuonyesha heshima kwa wazee, nawe umche Mungu wako.” (Walawi 19:32). Inaonekana kwamba kuheshimu wazee kulikwenda sambamba na heshima kwa Bwana Mwenyewe. Watoto wa umri wowote watapata amri hii katika Mithali: “Msikilize baba yako, aliyekuzaa, wala usimdharau mama yako atakapokuwa mzee” (Mithali 23:22). Timotheo wa Kwanza 5:1-2 inawahimiza waumini kuwachukulia wanaume na wanawake wazee kama baba na mama, jambo ambalo tunaweza kufungamanisha na amri ya Mungu katika Kutoka 20:12 ya kuwaheshimu baba na mama zetu. Biblia haitoi uhuru wa kuwadharau waliozeeka, haijalishi umri wao au uwezo walio nao.

Pia hatupaswi kupuuza kuwatunza wakongwe: “Kama mjane ana watoto ama wajukuu, hawa inawapasa awali ya yote wajifunze kutimiza wajibu wao wa kumcha Mungu katika matendo kwa kuwatunza wale wa jamaa zao wenyewe, na hivyo wawarudishie wema waliowatendea wazazi wao, kwa kuwa hivi ndivyo impendezavyo Mungu… Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini” (1 Timotheo 5:4,8). Hata katika uchungu Wake msalabani, Yesu alifanya mipango ya vile mamake atatunzwa, akimwomba mwanafunzi Wake Yohana amchukue kama mama yake mwenyewe (Yohana 19:26-27).

Ubaguzi dhidi ya wazee sio ubaguzi pekee wa umri unaozungumziwa katika Biblia. Paulo anamwagiza kijana Timotheo kuhusu umuhimu wa kuweka kielelezo kizuri: “Mtu yeyote asikudharau kwa kuwa wewe ni kijana, bali uwe kielelezo kizuri kwa waumini katika usemi, mwenendo, upendo, imani na usafi.” Wakati wa huduma Yake, Yesu aliwatumia watoto kama kiwango cha imani, usafi, na unyenyekevu tunaopaswa kutafuta (Mathayo 18:2-4).

Kutoka kwa haya yote tunaweza kuona kwamba ubaguzi wa umri ni kinyume na amri za Mungu kwa waumini. Huenda imani ya ubaguzi wa umri inaongezeka katika tamaduni zetu jinsi urembo, ujana, na ulimwengu unavyothamaniwa, lakini tunaweza kupigana nayo na kusimama kama mfano kupitia heshima yetu na kujali watu wa umri wowote.

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Je! Biblia inasema nini kuhusu ubaguzi wa umri?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries