settings icon
share icon
Swali

Je, Biblia inahusu nini?

Jibu


Kimsingi, Biblia inahusu mipango ya Mungu na makusudi ya ushirika wake na watu duniani. Mungu aliumba kila kitu, pamoja na watu ambao wameumbwa kwa mfano wake na ambao wameumbwa kwa kusudi dhahiri ya kuwa na ushirika naye.

Kitabu cha Mwanzo kinasimulia uumbaji wa watu wa kwanza, Adamu na Hawa, ushirika wao na Mungu katika Bustani la Edeni, kuanguka kwao katika dhambi, ambayo ilivunja ushirika huo. Matokeo ya uasi wa binadamu yalikuwa ni kifo na shida zilizoingia ulimwenguni. Ulimwengu hivi sasa hauko jinsi ulivyoumbwa; walakini, Mungu hakutupilia mbali Adamu na Hawa na uzao wao wote. Aliendelea kuwafuata na kuwavuta kwake licha ya dhambi yao.

Sura za mwanzo za kitabu cha Mwanzo zinaonyesha upotovu wa mwanadamu. Kaini alimwua ndugu yake Abeli. Ndani ya vizazi vichache, ulimwengu ulikuwa umearibika hivi kwamba Mungu aliamua kuangamiza kila mtu kwa mafuriko na kuanza upya na Nuhu na familia yake. Mungu alimwagiza Nuhu ajenge safina kuokoa familia yake na wanyama wengine. Hata baada ya mafuriko, Nuhu alionekana kuwa mtu mwenye dhambi pia. Idadi ya watu iliongezeka na ulimwengu wote ukakusanyika ili kujenga mnara "kufika mbinguni." Hii ilikuwa jaribio la wanadamu kumfikia Mungu kwa masharti yao yenyewe. Mungu hakupendezwa na alichanganya lugha zao ambazo ziliwatanya duniani.

Katika Mwanzo 12, Mungu alimchagua mtu mmoja, Abrahamu, na uzao wake kuwa njia ambayo ushirika kati ya Mungu na mwandamu utafanywa upya. Mungu aliahidi kwamba kupitia Abrahamu, ulimwengu wote utabarikiwa. Sehemu inayosalia ya Agano la Kale ni hadithi ya familia ya Abrahamu (taifa la Israeli) na mwingiliano wa Mungu nao. Mungu pia aliahidi Abrahamu nchi ya Kanaani kuwa urithi wa uzao wake.

Sehemu inayosalia ya Kitabu cha Mwanzo inasimulia hadithi ya makosa aliyofanya Abrahamu, mwanawe Isaka, na Yakobo,mjukuu wake (baadaye aliitwa Israeli), na wana kumi na wawiili wa Yakobo. Baadhi ya wana hao kumi na wawili waliuza Yusufu ndugu yao kuwa mtumwa kwa sababu ya wivu. Mungu alikuwa naye Yusufu na katika kipindi cha takriban miaka 20, Yusufu aliinuka kutoka utumwani na kuwa mtawala wa Misri, wa pili katika ngazi baada ya Farao. Basi kukawa na ukame na ndugu wa Yusufu wakaenda Misri kununua chakula na wanaungana tena na Yusufu, ambaye aliwasamehe na kuwahamisha wote kuenda Misri ambapo walipata chakula cha kutosha.

Kitabu cha Kutoka kinaanza karne kadhaa baadaye. Waisraeli wanaongezeka, na Wamisri kwa kuogopa idadi yao wanawafanya watumwa. Farao anaamuru watoto wote wachanga wa kiume wauawe. Mama mmoja anaficha mtoto wake kwa muda mrefu iwezekanavyo na kutengeneza kikapu kisiovuja maji na kumweka kwenye mto, karibu na mahali ambapo binti wa Farao huenda kuoga. Binti mfalme akapata kikapu hicho na kuamua kumweka mvulana huyo, ambaye anamwita Musa na kisha kumlea kama mjukuu wa Farao. Baadaye, Musa anapokuwa mtu mzima anaona ukandamizaji wa watu wake na kumuua Mmisiri amabaye alikuwa anampiga mtumwa Mwebrania. Farao anapata kujua kisha Musa analazimika kukimbia nchi na basi akawa mchungaji wa kuhamahama kwa miaka 40. Mungu akamtokea Musa na kumwambia arudi Misri na awaongoze watu kutoka utumwani. Musa anapoenda kwa Farao, Farao akakataa kukubaliana na matakwa ya Mungu. Basi Mungu anatuma mapigo mabaya juu ya Misri, ya mwisho ikiwa ni kifo cha mzaliwa wa kwanza katika kila familia. Walakini, mtu yeyote Mwisraeli au Mmisri ambaye alipaka damu ya mwanakondoo katika miimo miwili na kizingiti cha juu cha nyumba yake angeokolewa-hukumu ya Mungu itapita juu ya nyumba hiyo. Baada ya pigo la mwisho, Farao aliaambia watu waende na Musa akawaongoza kutoka. Walipofika kwenye ukingo wa Bahari Nyekundu, Farao alibadilisha nia yake na kuwafuata waliokuwa watumwa wake na jeshi lake. Mungu aliigawanya bahari na Waisraeli wakapita kati ya bahari kwenye nchi kavu, lakini maji ya bahari yakarudiana wakati Wamisri walipokua wanavuka na wakaangamia.

Kitabu cha Kutoka kinapoendelea, Musa anaanza kazi ya kuwaongoza Waisraeli kwenye nchi ambayo Mungu alikuwa ameahidi Abrahamu na kizazi chake. Walipokuwa njiani walipokea sheria ya Mungu ambayo iliwaambia jinsi ya kuishi kwa haki ili kumpendeza Mungu. Walipokea pia mipango ya maskani ( hekalu ya kuhamahama) ambapo wangekutana na Mungu. Katika kitabu cha Mambo ya Walawi Mungu alipatia Israeli maagizo juu ya ibada na dhabihu zilizohitajika kwa wenye dhambi kumwendea Mungu mtakatifu. Ingawa watu waliahidi kumtii na kumheshimu Mungu, kitabu cha hesabu kinaangazia kutofaulu kwao mara kwa mara. Kwa kweli, Waisraeli walikataa kuingia nchi ya Ahadi wakifikiri kwamba watu ambao walimiliki nchi hio walikua na nguvu sana kuwashinda. Kwa sababu ya kutoamini kwao, watu hao waliishi jangwani kwa takriban miaka 40 hadi kizazi kimoja kikakufa. Ndipo Mungu akawachukua watoto wao kwenye nchi hio. Kitabu cha Kumbukubu la Torati kina hotuba ya Mwisho ya Musa kwa kizazi kipya, ambao wengi wao hawakushudia ukombozi wa Miujiza wa Mungu kutoka Misri.

Kitabu cha Yoshua kinasimulia jinsi Waisraeli walivyoshinda na kuchukua Nchi ya Ahadi kupitia nguvu za Mungu. Kitabu cha Waamuzi kinasimulia maelewano yao ya kidini na ibada ya miungu ya uongo ya Kanaani. Mambo yaliyotendeka mara kwa mara ni kama uasi wa taifa, adhabu ya Mungu, kisha ukombozi kupitia jaji baada ya toba yao. Kitabu cha Ruthu kinasimulia hadithi ya mwanamke mwadilifu wa Moabu ambaye anajiunga na Israeli na kuwa nyanya-mkubwa wa Daudi, ambaye atakuwa mfalme mkuu wa Israeli.

Katika Samweli wa Kwanza tunapata hadithi ya nabii Samweli na jinsi alimtia mafuta mfalme wa kwanza wa Israeli, Sauli. Sauli alishindwa kwa sababu ya kutomtii Mungu, kwa hivyo Samweli alimtia mafuta Daudi. Daudi akawa msaidizi wa Mfalme Sauli, na mwishowe Sauli akashuku kwamba Daudi amechaguliwa kuwa Mfale, kwa hivyo akajaribu kumuua. Mwishowe Sauli aliuawa vitani na Daudi akawa Mfalme. Samweli wa Pili na 1 Mambo ya Nyakati vinasimulia juu ya utawala wa Daudi. Ingawa alifanya makosa mengi ya kushangaza, yeye alimpenda na kumheshimu Mungu. Mungu alimwahidi kwamba kila wakati atakuwa na kizazi cha kukaa kwenye kiti cha enzi.

Biblia pia ina seti ya vitabu vinavyojulikana kama fasihi ya hekima. Kitabu cha Ayubu kinaelezea hadithi ya mtu ambaye alipoteza kila kitu lakini akaendelea kumtumainia Mungu. Hoja ya kitabu cha Ayubu ni kwamba wakati mwingine watu waadilifu wanateseka bila sabau yotote -lakini Mungu daima ana sababu hata ikiwa hatotujulisha ni kwa sababu gani. Zaburi ni kitabu cha maombi/nyimbo/mashairi. Daudi aliandika kadhaa. Zinajumuisha nyimbo za sifa na maombi ya ukombozi kutoka kwa hatua nyingi za historia ya Israeli. Kitabu cha Methali ni mkusanyiko wa maneno ya busara na hekima ambayo yanahusihwa na Suleimani. Kitabu cha Mhubiri kinaelezea ubatilifu wa maisha ya Suleimani baada ya kumwacha Bwana. Kitabu cha Wimbo wa Suleimani ni hadithi ya mapenzi inayozungumzia raha za ndoa.

Vitabu za Wafalme wa Kwanza na wa Pili vinasimulia kuhusu wafalme waliofuata baada ya utawala wa Daudi. Mwanawe Suleimani alianza vizuri lakini akaingia kwenye ibada ya sanamu. Wakati mwanawe Suleimani alikuwa mfalme makabila kumi ya kaskazini yaligawanyika kutoka kwake, ikigawanya ufalme kuwa Kaskazini(Israeli) na kusini (Yuda), huku makabila ya Yuda na Benyamini wakibaki waaminifu kwa nasaba ya Daudi. Hakuna hata mmoja wa wafalme wa ufalme wa kaskazini aliyefuata Bwana, na ni wachache tu kutoka kusini waliomfuata. ( 2 Mambo ya Nyakati inasimulia mengi kuhusu wafalme wa Yudah au ufalme wa kusini.) Kulikuwa na nasaba nyingi kaskazini, lakini wafalme wote wa kusini walikuwa wazao wa Daudi.

Wakati wote wa wafalme, Mungu alituma manabii kuonya watu wake kwamba hukumu inakuja ikiwa hawatatubu dhambi zao. Hosea na Amosi walizungumzia ufalme wa kaskazini. Isaya, Yeremia (na Maombolezo, yaliyoandikwa na Yeremia), Yoeli, Mika, Nahumu, Habakuki, na Sefania walizungumzia ufalme wa kusini. (Obadia na Yona walizungumzia mataifa ya kigeni.) Hatimaye, watu hawakutubu na Mungu akatuma hukumu. Ufalme wa kaskazini uliharibiwa na Shamu takriban miaka 722 kabla ya Kristo, na ufalme wa kusini ulishindwa na Babeli mnamo 586 kabla ya Kristo. Yerusaleme na hekalu viliharibiwa na watu wengi wa Yuda wakahamishwa huko Babeli. Ezekieli na Danieli walikuwa manabii wa Mungu wakati huo wa uhamisho. Kitabu cha Esta kinahusu historia ya Wayahudi walioishi Uajemi wakati huo huo.

Baada ya Yuda kuwa uhamishoni kwa miaka 70, Mungu alianza kuwarudisha watu Yerusalemu ili kujenga upya. Nehemia na Ezra waliandika kuhusu wakati huo wa kujenga upya, na manabii Zekaria, Hagai, na Malaki walinena neno la Mungu kwa watu wakati huo. Daima, manabii walizungumza kuhusu ufalme uliorejeshwa, agano jipya, na uzao wa Daudi ambao ungetawala milele. Walianza kuashiria kwamba watu wa Mataifa (wasio Wayahudi) wangejumuishwa katika baraka hiyo. Lakini haikueleweka wazi jinsi mambo hayo yatakavyofanyika. Malaki ni nabii wa Agano la Kale, na baada yake kulikuwa na takiran miaka 400 bila hotuba ya unabii katika maandiko. Katika miaka hiyo 400, Israeli ilipata uhuru kwa muda mfupi kisha ikashindwa na Ufalme wa Kirumi.

Katika Injili za Agano Mpya (Mathayo, Marko, Luka, na Yohana) tunamuona nabii mpya, Yohana Mbatizaji, nabii wa kwanza katika karne nne, akitangaza kwamba ufalme umekaribia na Masihi atakayetawala anakaribia. Anatambulisha Masihi huyu kama Yesu. Vitabu nne vya injili vinasimulia kuhusu maisha na huduma ya Yesu. Ingawa alizaliwa Bethlehemu, hio haikuwa mwanzo wake kwa maana Yeye ni Mungu katika mwili wa mwanadamu aliyekuja kuishi kati yetu! Vitabu vya injili vinaonyesha miujiza yake na madai ya kimungu kama vile kudai kuwa sawa na Baba, kusamehe dhambi na kukubali kuabudiwa. Yesu alikusanya kikundi kidogo cha wanafunzi kumi na wawili kuongoza na kufunza. Aliwafunulia kuwa atauawa kulipia dhambi za ulimwengu. Hawakuelewa alichokua anasema wakati huo na alikataa wazo hilo. Je, Mfalme, Masihi, angeuawaje? Lakini kama alivyosema, Yesu alisalitiwa na kusulibiwa na kisha akafufuka kutoka kwa wafu. Badala ya kuanzisha ufalme wa kisiasa ulimwenguni, aliwaambia wanafunzi wake waeneze Habari njema ya maisha, kifo na ufufuo wake kwa ulimwengu wote. Yeyote anayemwamini yeye atasamehewa dhambi zake na kufanyika sehemu ya ufalme Wake. Yeye atarudi kwa nguvu wakati utakapofaa. Yeye anatimiza sheria ya Agano la Kale, na kwa sababu Yake hekalu na pia dhabihu na ukuhani zimepitwa na wakati. Atakaporudi, ufalme ulioahidiwa utazinduliwa.

Kitabu cha Matendo ya Mitume kinanakili kuja kwa Roho Mtakatifu na kuenezwa kwa injili ulimwenguni kote na wanafunzi wa kwanza (mitume), ispokuwa msaliti Yudasi na badala yake alikuweko Mathiya na mtume mpya aliyeitwa Paulo. Paulo alikuwa mtesaji wa kanisa, lakini Kristo alimtokea na kumpa agizo kuwa mtume kwa watu wa Mataifa.

Nyaraka za Agano Jipya ni barua zilizoandikwa na mitume kwa Wakristo katika maeneo tufauti ya Ufalme wa Kirumi, zikielezea mafundisho sahihi na kutaradhia tabia sahihi. Nyaraka kumi na tatu kati ya hizo zimeandikwa na Paulo, na majina yao inafafanua ni nani walioandikiwa: Warumi 1 na 2, Wakorintho, Wagalatia, Waefeso, Wafilipi, Wakolosai, 1 na 2 Wathesolanike ziliandikwa kwa makisa katika miji ya Korintho, Galatia, Efeso, na kadhalika; 1 na 2 Timotheo, Tito, Filemoni, ziliandikwa kwa watu binafsi. Barua hizi zote zinaelezea zaidi kuhusu Yes una jinsi injili inahusiana na maisha ya kila siku.

Nyaraka zingine zimepewa majina ya watu walizoziandika: Yakobo, 1 na 2 Petro, 1,2 na 3 Yohana; na Yuda. Aliyeandika waraka kwa Waebrania hajulikani, lakini umeandikwa kwa Waebrania (Wayahudi) ukielezea jinsi Agano la Kale imetimizwa katika Yesu.

Ufunuo ni kitabu cha mwisho cha Biblia. Mtume Yohana alikiandika kuelezea maono aliyoyapokea kutoka kwa Yesu. Kitabu cha Ufunuo kimejaa mifano ya kushangaza, lakini yote inaashiria kwamba Yesu atarudi na utawala wake utakuwa dhahiri bila kukanwa. Katika Yeye, ahadi zote kwa Abrahamu na kwa ulimwengu zitatimizwa. Wale ambao watamkataa watafukuzwa kwenda kwenye ziwa la moto. Ni kwa sababu ya maisha, kifo na ufufuo wake ndipo watu wanaweza kusamehewa na kuwa na ushirika naye Mungu ambao Adamu na Hawa walikua nao kisha kuupoteza. Baada ya yote, Mungu ataumba mbingu mpya na dunia mpya. Kilele cha hadithi ni Ufunuo 21:3: "Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao."

Biblia ni sakata ambayo inahusu historia yote ya mwanadamu. Hadithi ya Biblia niya ushirika wetu na Mungu ambao ulipotea hapo mwanzo, unarejeshwa kupitia huduma yake Kristo. Ushirika huu utapatikana kikamilifu katika mbingu na dunia zilizoumbwa upya, lakini kupitia Roho Mtakatifu, wale wanaoweka imani yao kwa Kristo wanaweza kufurahia kiwango cha ushorika huo hapa na sasa hivi.

Njia bora ya kujua Biblia ni kuisoma. Kama unaanza tu, unaweza kupata "hadithi" ya Biblia kwa kusoma vitabu vifuatavyo kwa mpangilio huu:
Mwanzo
Kutoka
Hesabu
Yoshua
Waamuzi
1 Samweli
2 Samweli
1 Wafalme
2 Wafalme
Ezra
Nehemia
Luka ( au vitabu vingine vya injili)
Matendo ya Mitume
Ufunuo

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Je, Biblia inahusu nini?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries