Swali
Je, kwa nini watu wengine hawamgeukii Mungu hadi baadaye Maishani?
Jibu
Ujumbe wa injili ni kwa vijana na wazee, kwa wanaume na wanawake wa kabila na tamaduni zote (Wagalatia 3:28). Lakini wengi wanaosikia ujumbe huwa hawajibu mara moja. Wengine huenda wasimgeukie Mungu hadi wanapozeeka.
Tukizungumza kwa ubinadamu, tunaweza kuwaza sababu nyingi za kutokumjibu Mungu hadi baadaye maishani-kuwa na familia au kazi, kutaka kusafiri, kufuatia idadi kadhaa ya michezo au shughuli za kijamii. Wengine wanaweza kudhani Mungu atangojea hadi maisha yao yatulie ndiposa wampe wakati. Wengine wanakiburi sana kana kwamba hawawezi kumkiri Mungu. Wengine wanaishi kwa raha kwa sababu ya juhudi zao na hawaoni haja ya kumgeukia Mungu. Wengine wanapenda dhambi zao. Wengine wana hakika kwamba wanapata wokovu wao kwa matendo mema, hawajamgeukia Mungu kwa imani.
Yesu aliongea kuhusu methali inayoonyesha watu tofauti wakiitwa kwa nyakati tofauti. Katika Mathayo 20:1-16 bwana wa shamba la mzabibu huajiri wafanyikazi kuleta mavuno. Wengine huanza kazi asubuhi na kukubali ujira wao. Mavuno ni mengi na bwana analazimika kuajiri wafanyikazi zaidi siku inavyoendelea hadi mwisho wa siku ya kufanya kazi. Bwana huyo anawalipa wale ambao walianza kazi mwishowe wa siku kiasi sawa na wale walioanza kazi mapema. Methali hii inazungumza kuhusu ukuu wa Mungu katika kuita yeyote atakaye, katika hatua yoyote maishani.
Tangu kabla ya uumbaji, Mungu alijua atakayemwita: "kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake" (Waefeso 1:4-5). Mungu anajua wakati sahihi wa kumwita mwenye dhambi kwa toba na wokovu. Wengi wanaweza kusikia wito wa nje wa wa Mungu, kwa kuwa mbegu ya neno la Mungu imemwagwa kote, lakini sio mbegu zote huanguka kwa "udongo mzuri" ambapo inaweza kumea na kutoa mavuno (Mathayo 13:1-23).
Kwa kuongeza, baada ya kusikia wito wa nje, watu lazima wasikie wito wa ndani wa Roho Mtakatifu kwani yeye ndiye anatuhukumu kwa dhambi zetu na kutuwezesha kuweka imani yetu katika Kristo (Yohana 16:7–15). Mfano wa wito huu wa ndani ni uongofu wa Lidiya. "Ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo" (Acts 16:14). Paulo alitoa wito wa nje, lakini Roho Mtakatifu ndiye aliyempa Lidiya wito wa ndani. Hatuwezi kwamwe kujibu vyema wito wa nje bila kwanza kujibu wito wa ndani wa Roho Mtakatifu. "Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni" ( 1 Wakorintho 2:14). Mungu ndiye anayetuvuta kwake; Yeye anaamua ni nani atakayemwita na lini atawaita. Wakati wake ni kamili.
Mpango wa Mungu kwetu umefichwa hadi Mungu atakapoamua kuufunua. Baada ya jambo kufanyika ndipo tunapoweza kuona jinsi Roho Mtakatifu alikuwa akifanya kazi kutuleta katika wokovu. Tunaweza kukumbuka jambo muhimu ambalo Mkristo alisema ambalo linatufanya kuwaza. Au pia tulitambulishwa kwa watu ambao maisha yao yalionyesha upendo na unyenyekevu wa Yesu. Labda hali zetu zilibadilika sana na kujipata katika hali ambayo hatukuchagua. Kupitia hafla zisizokusudiwa, mwishowe tukakubali kwamba tunakosa kitu muhimu, basi tukaanza kumtafuta Mungu na kuwa na hamu ya kuwa na uhusiano naye. Hadithi ya uongofu ya kila muumini ni ya kipekee, lakini jambo la kawaida ni kuwa Roho Mtakatifu anaongoza na Neno la Mungu kuzaa imani (Warumi 10:17).
Mungu anajua mioyo yetu na anajua ni nani atakayeitikia wito wake. Wakati kamilifu, Mungu huvunja vizuizi vyetu na wito wa ndani wa Mungu huwa haupingiki. Wale ambao hukataa wito wa nje, Roho wa Mungu hayuko ndani yao (Warumi 8:9).
Mungu hutuita lakini wakati mwingine huwa hatusikii. Mungu hutuita lakini wakati mwingine tunapuuza. Mungu hutuita lakini wakati mwingine kiburi chetu kinatuzuia. Wengine hungoja mkasa kutendeka ndiposa wachukue hatua ya kubadilisha maisha yao. Wengine hutambua mahitaji yao baada ya jambo kutendeka ambayo huwaleta kwa hatua ya unyenyekevu. Kwa sababu hizi na zinginezo, watu wengine huchukua muda kabla ya kufanya uamuzi wa kumgeukia Mungu. Hatari ya kuahirisha uamuzi huo ni kwamba wakati unaweza kuisha. Hakuna anayehakikishiwa kesho (Luka 12:20). Mungu ni mvumilivu , lakini baada ya kifo hakuna nafasi ya pili ya kuokolewa (Waebrania 9:27).
Wakristo wana jukumu la kueneza Habari njema, lakini ni Mungu ambaye huleta watu kwenye toba na imani ya kuokoa katika Yesu Kristo. Ikiwa kuna mtu unayemuombea, labda umemuombea kwa miaka mingi, fuata ushauri wa Yesu "omba na usikate tamaa" (Luka 18:1). Amini katika kubadilika na amini wakati wa Mungu.
Ikiwa unaahirisha wito wa Mungu wa wokovu, unacheza na moto. Wakati wa Mungu daima ni sasa (2 Wakorintho 6:2). Tunapopuuza wito wa Mungu tunajiweka kwa hatari ya milele.
English
Je, kwa nini watu wengine hawamgeukii Mungu hadi baadaye Maishani?