settings icon
share icon
Swali

Kwa nini fundisho la soli Deo gloria (Utukufu kwa Mungu pekee) ni muhimu?

Jibu


Soli Deo gloria ni mojawapo ya mafundisho muhimu yaliyosisitizwa wakati wa Matengenezo ya Kiprotestanti. Soli Deo gloria, Pamoja na solas zingine nne za Wanamatengenezo, hutenganisha injili ya kibiblia na Imani potofu. Neno la Kilatini soli humaanisha "pekee" au "tu" na maneno Deo gloria humaanisha "utukufu wa Mungu." Kwa hivyo, soli Deo gloria inamaanisha "Utukufu kwa Mungu pekee.

Soli Deo gloria inarejelea wokovu wetu katika Kristo. Wakati Wanamatengenezo walinena kuhusu wokovu wetu kuwa "kwa utukufu wa Mungu pekee," walisistiza neema ya Mungu. Wokovu ni kwa neema, sio kwa matendo yetu (Waefeso 2:8–9). Kifungu cha maneno muhimu katika Waefeso 2:9 ni "mtu asije akajivunia kitu", hivi kuwa, neema ya Mungu katika kutoa wokovu huondoa kiburi cha kibinadamu. Katika kutoa hoja yake ya kuhesabiwa haki kwa imani, mbali na sheria, Paulo aliandika, " Basi, tunaweza kujivunia nini? Hakuna! Kwa nini? Je, kwa sababu ya kutimiza sheria? La! Bali kwa sababu tunaamini" (Warumi 3:27).

Hakuna nafasi ya utukufu wa binadamu katika mpango wa Mungu wa wokovu. Utukufu ni wa Mungu peke yake. Yesu alisema, "pasipo mimi hamwezi kufanya neno lolote" (Yohana 15:5). Ikiwa ingewezekana kwa mtu kupata wokovu kupitia kazi za sheria, basi angekuwa na kitu cha kujivunia (Warumi 4:2); lakini haiwezekani. Hatuwezi kujiokoa. Sisi ambao tulikuwa wafu kwa sababu ya dhambi zetu (Waefeso 2:1) hatungeweza kufanya lolote kujisaidia kupata uzima. Lakini, asifiwe Bwana, "karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu" (Warumi 6:23). Utukufu ni wa Mungu, sio wetu. Soli Deo gloria.

Wokovu wa wenye dhambi ulikuwa ni wazo la Mungu, kukamilika kwa wokovu huo kulikuwa ni kazi ya Mungu, kutoa wokvu huo ni neema ya Mungu, na kutimizwa kwa wokovu huo ni ahadi ya Mungu. Kuanzia mwanzo hadi mwisho, "Mwenyezi Mungu ndiwe uokoaye" (Zaburi 3:8; linganisha na Ufunuo 7:10). Yesu alifananisha wokovu na kuzaliwa upya (Yohana 3:3); kwa kuwa mtoto mchanga hawezi kuchukua sifa kwa kuzaliwa kwake mwenyewe, basi hatuwezi kuchukua sifa kwa "kuzaliwa tena" kwetu. Mfalme Hezekia hakusifiwa kwa wokovu wa Yerusalamu kutoka Waashuri (2 Wafalme 19); Mungu ndiye aliyemshinda adui. Shadraka, Meshaki na Abednego hawakusifiwa kwa kujiokoa kutoka kwa tanuru la moto (Danieli 3); Mungu aliwaifadhi ndani ya moto. Utukufu ni kwa Mungu pekee. Soli Deo gloria.

Katika theolojia ya Mageuzi, funzo la soli Deo gloria linakaribiana na funzo neema isiyoweza kuzuiliwa. Neema ya Mungu ilituvuta kwa wokovu na hata kutuweza kuamini. Naam, tunatubu dhambi zetu, lakini ni kwa sababu neema ya Mungu inatuwezesha kutubu. Tuliweka Imani yetu kwa Kristo, lakini ni kwa sababu neema ya Mungu ilituwezesha kuwa na imani. Hakuna kazi tunaweza kufanya kwa namna yoyote ili tupate wokovu au kutusaidia kuupata kwa ajili yetu. Tumeitwa na kulindwa na nguvu ya Mungu pekee "Ndivyo alivyopenda kuonesha kwa watu wa nyakati za baadaye ukuu wa neema yake aliyotujalia kwa ukarimu katika kuungana kwetu na Kristo Yesu" (Waefeso 2:7). Soli Deo gloria.

Mtunga nyimbo wa Ujerumani Johann Sebastian Bach (1685-1750) alielewa kuwa nyimbo zilikuwa karama kutoka kwa Mungu na hutumika kwa utukufu wa Mungu. Katika utunzi wake wote wa nyimbo za injili, Bach aliandika herufi za kwanza za jina SDG, soli Deo gloria. Katika ndoto yake ya mbinguni mtume Yohana aliona "wale wazee ishirini na wanne hujiangusha mbele ya huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi na kumwabudu huyo ambaye anaishi milele na milele; na huziweka taji zao mbele ya kiti cha enzi wakisema: "Wastahili ee Bwana na Mungu wetu, kupokea utukufu na heshima na nguvu. Maana wewe uliumba vitu vyote, na kwa matakwa yako viliumbwa na vipo.'" (Ufunuo 4:10-11). Hata wazee wa mbinguni hawavai taji zao; wanatoa utukufu kwenye kunastahili-kwa Mungu pekee.

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Kwa nini fundisho la soli Deo gloria (Utukufu kwa Mungu pekee) ni muhimu?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries