settings icon
share icon
Swali

Ni kwa nini ni muhimu kumshukuru Mungu?

Jibu


Biblia imejaa amri za kumshukuru Mungu (Zaburi 106:1; 107:1; 118:1; 1 Mambo ya Nyakati 16:34; 1 Wathesalonike 5:18). Vifungu vingi huendelea na kuorodhesha sababu za ni kwa nini tunapaswa kumshukuru kwa kuwa “Fadhili zake zadumu milele” (Zaburi 136:3), “Yeye ni mwema” (Zaburi 118:29), na “huruma zake ni za milele” (Zaburi 100:5). Shukrani na sifa daima huenda pamoja. Hatuwezi kumsifu na kumwabudu Mungu vya kutosha bila kumshukuru.

Kuhisi na kuonyesha shukrani ni vizuri kwetu. Kama baba yeyote mwenye hekima, Mungu anataka tujifunze kushukuru kwa zawadi zote ambazo ametupatia (Yakobo 1:17). Ni kwa manufaa yetu kukumbushwa kwamba kila kitu tulicho nacho ni zawadi kutok Kwake. Bila shukrani, tunakuwa wenye kiburi na wenye ubinafsi. Tunaanza kuamini kuwa tumefanikiwa kwa kila kitu kupitia juhudi zetu wenyewe. Shukrani huiweka mioyo yetu katika uhusiano mzuri na Mpaji wa zawadi zote nzuri.

Kutoa shukrani pia hutukumbusha kiasi tuko nacho. Wanadamu huwa na tabia ya kutamani. Kuna mazoea ya kuangazia kile ambacho hatuna. Kwa kuendelea kutoa shukrani tunakumbushwa kiasi ambacho tuko nacho. Tunapoangazia baraka badala ya mahitaji tunakuwa na furaha zaidi. Wakati tunaanza kumshukuru Mungu kwa mambo ambayo huwa tunayachukulia kuwa ya kawaida, mtazamo wetu hubadilika. Tunatambua kwamba hatungeweza hata kuwepo bila baraka za rehema za Mungu.

Waraka wa kwanza wa Wathesalonike 5:18 inasema, “shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu.” Tunapaswa kushukuru sio tu kwa vitu tunavyopenda, lakini kwa hali ambazo hatupendi. Tunapokusudia kumshukuru Mungu kwa kila kitu anachoruhusu kitendeke katika maisha yetu, tunazuia uchungu. Hatuwezi kuwa na shukrani na uchungu kwa wakati mmoja. Hatumshukuru kwa mabaya, bali kwamba yeye anatudumisha katika maovu (Yakobo 1:12). Hatumshukuru kwa madhara ambayo hakusababisha, lakini tunamshukuru anapotupa nguvu za kuyastahimili (2 Wakorintho 12:9). Tunamshukuru kwa ahadi yake kwamba “mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao, katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake” (Warumi 8:28).

Tunaweza kuwa na mioyo yenye shukrani kwa Mungu hata wakati hatuhisi shukrani kwa ajili ya hali ilivyo. Tunaweza kuhuzunika na bado kuwa na shukrani. Tunaweza kuwa tumeumia na bado tuwe na shukrani. Tuanweza kukasirikia dhambi na bado tuwe na shukrani kwa Mungu. Hiyo ndiyo Biblia inaita „dhabihu ya sifa” (Waebrania 13:15). Kutoa shukrani kwa Mungu huweka mioyo yetu katika uhusiano mzuri na Yeye na hutuokoa kutoka kwa hisia nyingi zinazoweza kudhuru na mitazamo ambayo itatunyang’anya amani ambayo Mungu anataka tuipate (Wafilipi 4:6-7)

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Ni kwa nini ni muhimu kumshukuru Mungu?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries