settings icon
share icon
Swali

Je, ninawezaje kupata shauku ya kuvuta nafsi kwa Kristo?

Jibu


Kuvuta nafsi, kwa hakika ni mchakato wa kufanya uinjilisti au kushuhudia, ambayo kwa kwa ufupi ni kuwasilisha ujumbe wa wokovu kwa wasioamini. Yesu Kristo aliwaambia wanafunzi Wake kwamba wawe mashahidi Wake hadi “miisho ya dunia” (Matendo 1:8) na “enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi” (Mathayo 28:19), ambayo ndiyo kiini cha kupata nafsi. Kama vile Baba yetu wa mbinguni hapendi mtu yeyote apotee (2 Petro 3:9), Wakristo wote wanapaswa kuwa na shauku ya kutii wito huu na kuwa na shauku ya kupata nafsi.

Kushuhudia, hata hivyo, sio kile tufanyalo kwa ajili ya Bwana, bali ni kile afanyacho kupitia kwetu, na hii inahitaji moyo uliosalimishwa na uliojazwa na Roho Mtakatifu. Hakika, Roho Mtakatifu yule yule aliyemtia nguvu Kristo alipokuwa akihudumu duniani anaweza kututia nguvu pia. Ingawa kwanza tunahitaji kuelewa jukumu letu katika kuujenga mwili wa Kristo. Kama vile mtume Paulo alivyowaeleza wale wa Korintho, sisi ni watumishi wa Mungu wanaofanya kazi kwa umoja ili kuzalisha mavuno. Mmoja atalima udongo, mwingine atapanda mbegu, na mfanyakazi mwingine ataimwagilia maji, lakini ni Mungu pekee anayeweza kuikuza mbegu hiyo (1 Wakorintho 3:7). Kwa hivyo, ingawa kila mmoja wetu anaweza kuwa na majukumu binafsi, hata hivyo tuna lengo moja la kuwaleta wengine kwa Kristo, ambako kila mmoja atapokea thawabu yake mwenyewe kulingana na kazi yake mwenyewe (1 Wakorintho 3:8).

Je, ni namna gani tunaweza kupata shauku ya kueneza habari hii njema na kupata kuleta nafsi nyingi kwa Kristo katika siku hizi ngumu wakati kuna wengi wanaopinga kazi yetu kila hatua? Inaanza na kumtanguliza Yesu Kristo na kuwa kiini cha maisha yetu. Hakika, shauku yetu ya kuleta nafsi kwa Kristo itaongezeka kadri shauku yetu kwa Kristo Mwenyewe na matembezi yetu pamoja Naye yanavyozidi kuwa na nguvu. Njia mbili bora za kuimarisha matembezi yetu ya Kikristo ni kusoma Neno Lake kila siku na kuomba bila kukoma. Tunapojaza mioyo yetu na akili zetu na Kristo, hatuwezi kujizuia kuwa na shauku ya kumweneza kwa wengine.

Watenda kazi wenye shauku ni wale wako na moyo unaowaka moto kwa ajili ya Kristo, na hii inapaswa kuwa rahisi tunapozingatia ukubwa wa kile Mwokozi asiye na dhambi alitufanyia pale Kalvari. Kukubali kwake kifo kwa hiari kwa niaba yetu kulituponya kutokana na ugonjwa wetu wa mwisho (dhambi) na kutuokoa kutoka kwa umilele usiopimika katika ziwa la moto. Lakini tunajua kile kinachowatokea wale wanaokufa bila Kristo. Na umilele huu usio na tumaini mbali na Mungu, sembuse katika giza la moto usiozimika jahanamu, inapasa kututia moyo katika kuleta nafsi nyingi kadri tuwezavyo, haswa tunapofikiria ufupi wa maisha ambao mtume Yakobo anauita vile unavyofaa “Ninyi ni ukungu ambao huonekana kwa kitambo kidogo kisha hutoweka” (Yakobo 4:14). Pindi tunapovuka upeo wa milele, hakuna kurudi nyuma, na wakati wa kuvuta nafsi utakuwa umekwisha. Hivyo, sio eti mavuno ni mengi pekee na wafanyikazi ni wacheche, bali ni zaidi ya hilo, muda wetu ni mfupi.

Katika nyakati hizi zenye changomoto, hakika hatuhitaji kutazama mbali ili kuona wengi wakiwa wamekata tamaa, hata hivyo, hata katikati ya machafuko haya, Wakristo wanaweza kupata kitulizo katika Neno la Mungu. Kwa mfano, Mkristo akijikuta katika mojawapo ya majaribu maishani, anajua kwamba Bwana wetu Mkuu ndiye alimweka hapo au anamruhsu awe huko. Vyovyote iwavyo, Mkristo anaweza kupata maana ya msukosuko huu kwa kutambua kwamba Mungu ana kusudi kwa ajili ya majaribu yetu, kwa maana tunajua kwamba “katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wampendao” (Warumi 8:28). Zaidi ya hayo, ikiwa maisha mara kwa mara hayana maana kwetu ni sawa, kwa kuwa tunajua kumtumaini Bwana kwa mioyo yetu yote na kutotegemea ufahamu wetu wa hali fulani (Mithali 3:5-6). Kuvumilia magumu ya maisha ambayo hutujia bila kuepukika ni rahisi wakati tunajua kwamba Mungu ndiye anayetawala.

Nafsi karibu nasi zilizopotea zinaweza kupata faraja hii wakati wanaiweka imani yao kwa Kristo. Ingawa, vile Paulo alivyoelezea, “Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria? Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri habari njema!” (Warumi 10:14-15). Amani ya Mungu, ambayo inapita fahamu zote na kulinda mioyo yetu wakati wa nyakati ngumu (Wafilipi 4:7), inaweza kulinda nyoyo zao pia, pindi wanapomruhusu kuingia ndani yao.

Hakutakuwa na mwito mwingine bora zaidi kuliko kufanya kazi kwa niaba ya Yule aliyekufa ili tupate kuishi. Yesu alisema, “Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru” (Yohana 15:14), na amri zake zilikuwa kuwa tumtii Yeye na kwamba tupendane sisi kwa sisi jinsi alivyotupenda. Kwa wazi, basi, upendo wetu Kwake unadhihirishwa wakati tunamtumikia kwa bidii na bila kuchoka kushiriki injili Yake na wengine.

English



Rudi kwa ukurasa wa nyumbani wa Kiswahili

Je, ninawezaje kupata shauku ya kuvuta nafsi kwa Kristo?
Shiriki ukurasa huu: Facebook icon Twitter icon Pinterest icon Email icon
© Copyright Got Questions Ministries